Unaona Nini?

Maandiko yanatuambia katika  Biblia Takatifu

Mith 23:7a “Aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo”.

Je wewe unaona nini mbele yako? Siku zote huwezi kuona kwenye moyo wako tofauti na kile unachokula kwa kusikia, kutazama ama kuhisi

Hii ndio sababu ninashauri watu wajifunze kuwa na vitu positive wanavyojishugulisha navyo kila siku kwenye maisha yao, maana kama wewe unasikia mambo ya mauti, unaona mambo ya mauti, unahisi mambo ya mauti ni rahisi kuota hata umekufa au uko kwenye jeneza ukasema nguvu za giza kumbe nafsi yako imejaa ayo mambo .

Marafiki wanaokuzunguka wanajaza nini kwenye nafsi yako, maana wanachokijaza kitakuwa na mchango mkubwa katika mtazamo wako kimaisha , mazingira yanayokuzunguka yanajaza nini katika nafsi yako, filamu unazo anagalia zinajaza nini, nyimbo unazo sikiliza mara kwa mara zinajaza nini katika nafsi yako, maana kama unakaa na watu waliokata tamaa uwe na uhakika hata maisha yako yatakuwa ni ya kukata tamaa tu.

Kama wewe ni mwana ndoa na mda mwingi unautumia kukaa na walioachika unaweza ukajikuta umeanza kubadilika kimtazamo, Ndio sababu Biblia ikasema katika;

1 Timoth 4:16 “Jitunze nafsi yako na mafundisho yako…”

Unajitunzaje ni kwa kuwa makini na vitu utakavyokuwa ukiviruhusu kuingia katika nafsi yako, kumbuka kuona kwako, kesho yako itategemea nini unakipa nafasi katika nafsi yako leo.

Waabuduo Katika Roho Na Kweli

Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

https://www.facebook.com/efathambinga
Wana wa Mungu wakimfanyia Mungu wao Ibada.

Si matendo yote ya ibada ambayo Mungu anayakubali, kwa sababu si wote wamwabuduo ni waabudu halisi. Ukweli huu ulifunuliwa na Yesu alipokuwa anafanya mazungumzo na mama Msamaria katika kisima cha Yakobo. Alifunua pia ukweli mkubwa juu ya ibada ambayo tunatakiwa kuzingatia sana endapo tunataka ibada yetu ikubalike na Mungu.

Jambo la kwanza kuelewa ni kwamba kila “Mungu” ambaye anapatikana eneo fulani tu si Mungu wa kweli na hatakiwi kuabudiwa. Ibada inayofanyika kwa Mungu wa namna hii ni ibada feki. Ibada ya Mungu wa kweli haihusiani na kwenda njiapanda ambapo barabara tatu zinakutana kuweka chakula ili Mungu aje ale. Mtume Paulo alikutana na waabuduo namna hii katika milima ya Mars huko Athene (Matendo ya Mitume 17:22-31). Mungu wa Kweli anaelezewa na Mtunzi wa Zaburi katika Zaburi 8:1

Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;”

Ukweli mwingine ambao Bwana Yesu alitufunulia ni kwamba mungu yeyote ambao hana mahusiano ya ubaba na waabuduo huyu hastahili kuabudiwa nasi. Mtu yeyote anayemwabudu Mungu kwa namna hii si mwabudu halisi. Ndiyo maana Yesu alikuja kutufanya sisi wa Baba Yake. Na hata alipokuwa anawafundisha wanafunzi wake namna ya kuomba, alimwelezea Mungu wa kweli kama “Baba” (Luka 11:2). Zaidi sana, Bwana Yesu alitufunulia kuwa ibada yetu kwa Mungu si halisi kama hatumjui Mungu tunaye mwabudu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo kuwatambulisha watu wa Athene kuwa walikuwa wanaabudu kwa ujinga (Matendo ya Mitume 17:23). Alijaribu kuwafundisha kwamba ni kosa kumwakilisha kichwa cha Mungu na dhahabu, fedha, au jiwe lililo chorwa kisanaa na vitu vya kibinadamu (Matendo ya Mitume 17:29). Hakuna mwabudu ambaye kwa ujinga akafikiri kuwa Mungu Mtakatifu atakubali ibada toka kwa mtu ambaye maisha yake yametawaliwa na dhambi za uongo, kujifanya na kila aina ya maadili mabaya na uovu.

Ibada ya kweli inahusiana na kumwabudu Mungu wa kweli katika roho na kweli. Lazima tumwabuduo Mungu katika roho kwa sababu Mungu ni Roho, na ni kwa roho pekee tunaweza tukaendana na Roho Yake. Kumwabudu Mungu katika roho ina maana kufanya kile anachokuagiza ufanye katika akili ya kiroho ya imani. Kuna mambo ambayo Roho Mtakatifu wa Mungu angetaka sisi tufanye lakini tungeliona kwa macho yetu ya kimwili, ni magumu kuyaelewa. Kwa mfano, pale Mungu alipo muagiza Nuhu kujenga safina kubwa sana katika nchi kavu, kwa watu wa kizazi chake, hili halikuwa jambo lenye maana la kulifanya. Kwamba mtu lazima awe na mme au mke mmoja “haijarishi pana ubaya au wema” watu hawaoni umuhimu lakini ndivyo Mungu wetu atakavyo katika Neno lake. Mwabudu halisi hataweza kusema uongo hata kama kuna madhara yanayoweza kumpata kupitia Ukweli wake. Kwa mwabudu halisi kuwa mkweli si kwa ajili ya mtu bali kwa Mungu ajuaye yote.

Yohana 4:21-24 “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Ombi la Msingi: Baba neema ya kuishi maisha yanayokunalika kukuabudu wewe kupitia Roho Mtakatifu wako, katika Jina la Yesu.

Usifumbe mdomo II

Yohana 15:16 “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”

PastorBoniface
Mchungaji Boniface akiwa kazini.

Ni kazi yetu kama wana wa Mungu kufungua midomo yetu kwa mapana kwa hiki kizazi kilichopotoka na kuwafundisha mausia ya Mungu bila hofu au haya ama upendeleo. Kwa kuongezeka katika somo lile la Usifumbe mdomo I. Katika kufungua midomo yetu kwenye maombi, kufungua midomo yetu kama mashahidi ya Bwana Yesu ni wajibu mwingine ambao lazima tuufanye uinjilishaji wa kuwafikia wenye dhambi ni kwa ajili ya kila mwana wa Mungu; si kwa watumishi wa madhabahuni tu. Lazima wote tuzae matunda ya roho kama tulivyosoma hilo Neno la leo.

Kuturudisha katika huu wajibu Bwana wetu Yesu Kristo anatuthibitishia kwamba nguvu zote mbinguni na duniani ni zake. Hivyo ni jambo lililotulia sana kwamba hakuna kinachoweza kutuzuia sisi hapa duniani na ulimwengu wa roho kubeba maagizo ya Bwana. Hivyo hatuwezi kusamehewa endapo tutashindwa kuokoa roho za watu. Ametuagiza kwenda kufundisha mataifa yote, tukiwabatiza kwa jina la Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Hivyo utume mkuu tuliochaguliwa tuufanye ni pamoja na kufundisha. Acha tutulie na kuwaza kwamba hivi hili zoezi la kufundisha lina maana gani hasa?

Kufundisha ni kusema Ukweli ambao utapelekea mabadiriko kwa afundishwaye. Tunapambana na matatizo makuu mawili katika Utekelezaji wa utume huu. Moja ya haya matatizo ni uoga wa Mwalimu anayetakiwa kufundisha endapo mwanafunzi atakuwa na upinzani wa mabadiriko, hivyo huamua kufumba mdomo (kunyamaza). Lakini Biblia inatuambia katika 2 Timotheo 4:2

lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.”

Tatizo la pili, ni kwamba watu Wanaotakiwa kufundishwa hawako tayari kufurahia kilio cha “mabadiriko”. Hawako tayari kutishwa na “fanya haya na usifanye haya” yatokanayo na imani mpya ndani ya Yesu Kristo. Watu wa namna hii hujiangamiza wenyewe kwa sababu wanasema hatujaitwa kuwa chini ya sheria. Uhalisia ni kwamba Haijalishi tunakubali ama tunakataa, nira ya “kujifunza na kubadirika” imeambatanishwa katika wito wetu katika imani. Bwana wetu Yesu Kristo alisema katika Mathayo 11:29a:

Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu

Ni kazi yetu kama wana wa Mungu kufungua midomo yetu kwa mapana kwa hiki kizazi kilichopotoka na kuwafundisha mausia ya Mungu bila hofu au haya ama upendeleo.

Kuna mahali fulani kanisani nilimsikia dada mmoja akifundisha Kuhusu utoaji wa zaka [fungu la kumi]. Ili kuwafanya watu watu wakubali fundisho lake alisema unaweza kuanza kwa kutoa 5% ya mapato yako kisha watazidi kuongeza taratibu. Hili ni kosa kubwa sana katika mafundisho ya Neno la Mungu, hatutakiwa kupunguza Neno au kuongeza Neno tufundishe Ukweli ambao tumetumwa. Hii ndiyo njia pekee ya kuyafanya matunda yavumilie, na maombi yetu yatajibiwa.

Mathayo 28: 18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; 20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Jambo la Kuzingatia: Amua kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wa Yesu kupitia ufundishaji wa Neno la Mungu kama lilivyo katika Biblia kuanzia leo.

Usifumbe mdomo I

Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!”

Daniel, mtu mkuu wa maombi, akiliombea taifa lake, Israeli. Katika maombi yake alimuomba Mungu kulikumbuka agano lake la kurejesha taifa la Israeli. Aliadhimia kuutafuta uso wa Bwana kwa rehema, kupitia maombi na dua pamoja na kufunga. Aliomboleza kwa kudaharauliwa kwa Wayahaudi waliokuwa wametawanyika dunia nzima na kwa uharibifu wa mji wa Yerusalem. Tunajifunza jambo kubwa sana kwa maisha yetu ya leo tunapotafakari maosha ya Danieli.

Moja ya funzo kubwa tunalipata katika sentesi hii “..mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu…” (Danieli 9:2). Ulikuwa ni ugunduzi na ufahamu wa Danieli kulijua Neno la BWANA alilolisema kupitia Nabii Yeremia katika Yeremia 29:10, juu ya muda wake wa kuja kuirejesha Israeli taifa ambalo lilimsukuma kuwaombea watu wake.

Elewa Ukweli kwamba katika wakati huu, hakukukuwa na Biblia inayounganisha maandiko ya manabii pamoja kama leo. Maandiko ya manabii yalikuwa katika vitabu tofauti vilivyotawanyika katika maeneo tofauti tofauti. Hivyo ilikuwa ni kazi nzito sana kwa Danieli kumtafuta vitabu husika cha manabii, na kisha kuvisoma vyote ili afike mahali pa kujua BWANA alisema nini juu ya hali waliyokuwa wamechoka nayo. Kusoma, kujifunza na kutafakari juu ya Neno la Mungu ni kazi ngumu sana, japo kwa kiwango kile utavyokuwa umefahamu Biblia ni kwa kiwango hicho utapata kujua akili ya Mungu Kuhusu wewe. Ukishajua akili au wazo la Mungu kuhusiana na hali fulani, itakujengea ujasiri wa hali ya juu sana unapomwendea BWANA kwa maombi.

Bwana wetu Yesu Kristo alituhakikishia juu ya kujibiwa kwa maombi yetu katika Mathayo 7:8. Alilisitiza uhakika huu kwa kauliza swali hili katika Mathayo 7:9

Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?

Kulijibu swali la Bwana wetu Yesu, baba hakika hawezi kufanya hivyo. Mara ngapi zaidi Baba yetu wa mbinguni aliye mwema kuliko baba zetu wa duniani (Mathayo 7:1)? Hivyo nakusukuma kusoma vitabu ili uweze kujua akili au mpango wa Mungu, ili uweze kuomba vema muda wote. Hili peke yake linakupa dhamana ya kupata majibu ya haraka kwa kila maombi ya mahitaji yako. haitakuwa vizuri kwako kuingia katika maombi yasiyo kuwa na maana. Omba sawasawa na akili au Mawazo ya Mungu yaliyo wazi katika Neno lake Takatifu na utaona furaha ya maombi yako. usigunge mdomo wako na kuugua kwa ukimya.

Danieli 9:1-19 “Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; 2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. 3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. 4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; 5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; 6 wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. 7 Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. 8 Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. 9 Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; 10 wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii. 11 Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi. 12 Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu. 13 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba Bwana, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. 14 Basi Bwana ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. 15 Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. 16 Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. 17 Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. 18 Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi. 19 Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.”

Omba: Baba wa Mbinguni, wasaidie viongozi wa nchi yangu ya Tanzania kuwa na uhai kwenye majukumu yao, katika Jina la Yesu.

Ni Kwa Ajili Ya Mema Yako

Tangu mwanzo, namna ambavyo shetani anafanya kazi amekuwa akipanda mbegu ya mashaka katika mioyo wa watu ambao Mungu amewawekea mpango maalum na kusudi la Mungu kwao. Mfano, wakati lengo la Mungu kumkataza Adam na Eva wasile tunda lililokatazwa lilikuwa ni kuwafanya waishi milele, wenye afya na ustawi, shetani akawaendea na kuwaambia eti Mungu kawakataza kwa sababu hawataki mema (Mwanzo 3:4-5).

Ni aina hii ya mashaka ambayo shetani alipanda kwa ndugu zake Yusufu baada ya kifo cha baba yao. Ashukuriwe Mungu Yusufu alikuwa mtu anajua Mawazo ya Mungu; akawazima mashaka yao mara moja. Kwa sisi wana wa Mungu siku hizi, Mungu ametufunulia mpango wake na makusudio yake kwetu katika Yeremia 29:11:

Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Hili si wazo jipya kwa Mungu, isipokuwa hili limekuwa kusudio la Mungu kwengu tangu mwanzo wa uumbaji (Mwanzo 1:26). Elewa kuwa ni dhambi kuwa na mashaka dhidi ya mema katika nia ya Mungu. Anapotuongoza kufanya jambo au kuishi kwa namna fulani ambayo ni kinyume na namna ambayo shetani au watu wanatutegemea sisi kuishi kwayo.

Kwa kuwa Yusufu alifahamu Mawazo ya Mungu kuhusiana na yote yaliyomtokea alikataa kufanya ibada ya mashujaa kutoka kwa ndugu zake na akatuliza mashaka yao. Aliwafariji kwa kuwafanya waelewe kuwa matendo mabaya waliyomfanyia yalitokana na Mungu ili akamilishe kusudi lake katika maisha ya Yusufu.

Mwanzo 50:19-20 “Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? 20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.”

Kwa lugha nyingine Yusufu alikuwa anawaambia ndugu zake kuwa haikuwa wao ila Mungu aliyemtuma yeye Misri kwa kusudi lililo wazi sana. Ndiyo maana Mtume Paulo akasema;

Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

Bwana anasema na wewe kuwa acha kulalamika Kuhusu nini kinatokea kwako leo; ni kwa ajili ya mema yako. Mambo yako yatakuja kuwa mazuri sana endapo utaendelea kumpenda Mungu hata kama utakuwa katika hali mbaya sana, ambayo ina kusudi la kiungu. Narudia tena kukuambia wewe: ni kwa ajili ya mema yako, na muda si mrefu utajua ni kwa nini.

Mwanzo 50:15-21 “Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. 16 Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, 17 Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. 18 Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. 19 Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? 20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. 21 Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.”

Omba: Baba, kutokana na Neno lako, mambo yote yafanyike mema kwa kusudi lako juu yangu, katika Jina la Yesu.