Uzao Mteule na wa Kipekee

cropped-bon22
Mchungaji Boniface Evarist, akifundisha Neno la Mungu

 

1 Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu”

Mkristo ni uzao mteule wa Mungu ambaye ndani yake amempokea Roho wa Kristo. Kristo ni cheo cha juu sana katika ufalme wa Mungu. Ikumbukwe kuwa hata Yesu hakupewa jina hili la Kristo mpaka aliposhinda kifo na mauti na kuikamilisha kazi ya Ukombozi wa mwanadamu aliyekusudiwa na Mungu; hapo ndipo Biblia inasema katika Wafilipi 2:9-11:

Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; 11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Mungu amekuita wewe kutoka kwenye maisha ya dhambi na amekuingiza kwenye pendo lake Umekuwa raia wa Mbinguni lakini ni balozi wa Mbinguni hapa duniani. Hivyo tambua kuwa una cheo cha KRISTO ndiyo maana unaitwa Mkristo maana yake mpakwa mafuta wa BWANA.

Kuna sifa nyingi zinazoonesha kuwa wewe ni Uzao mteule na wa kipekee. Maana uzao wa kipekee:

  • Ni wale wanaomtafuta Bwana, kila siku wanautafuta uso wa BWANA (ZABURI 24:6).
  • Uzao wa kipekee ni watu waliopokea rehema za Mungu na kupitia ile rehema wamepata neema ya kuwa watatuzi wa kila matatizo wanayowasumbua watu na waondoa kila vizuizi vya ustawi.
  • Ni uzao wa watu ambao hawazuiliwi na chochote. Tunayo mifano Mingi katika Biblia, mfano Yusufu alikuwa wa uzao huu licha ya mapito mengi aliyopitia akaweza kuwa kiongozi bora na mtatuzi wa matatizo ya mataifa na kuishia kuwa waziri mkuu wa kwanza akiwa utumwani.

Ili uweze kuwa mmoja wa kundi hili la uzao mteule lazima ukubali kumuona Mungu katikati ya kundi la wengi wasiomuona na kumwamini Mungu. Kama Paulo alivyosema

17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike.” (2 Wakorintho 6:17-18).

Ukiweza kutoka kwenye utamaduni wao, mila zao, desturi zao, imani yao namna yao ya mtindo wa maisha ukaacha. Ukafuata kile NENO LA MUNGU limesema wewe utakuwa MKRISTO wa kweli na ile ROHO YA KRISTO itafanya kazi ndani yako na hapo ndipo utasema nafanana na Yesu na utafanya kama Yesu au zaidi ya Yesu mwenyewe maana alisema

Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.”

Daima Ubarikiwe Msomaji

Mch. Boniface Evarist.