Maombi Na Uponyaji

Ibada ya Jumapili Juni 28, 2015.

Mwanzo 20:17-18 “Ibrahimu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. 18 Maana Bwana alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.”

Tunaona kwa mara ya kwanza mwanadamu ana muombea mgonjwa, hapa Ibrahim aliombea kwa ajili ya Abimeleki na Mungu akaleta Uponyaji kwa nyumba yote.

Magonjwa mengi yanaruhusiwa na Mungu Mwenyewe. (Yeremia 30:12-17 “….”) Mara nyingi chanzo cha matatizo ya kiafya ni tabia zetu sisi wenyewe Ukisoma hapo anasema nimekutenda haya ya afya mbaya kisa maovu yako. Kazi yako ni kujichunguza je mimi niko sawa na Mungu? Unaweza sema umeokoka lakini bado unalewa, unasengenya, unaweza vibaya, unazini kwa jinsi hiyo Mungu haponyi mtu na kamwe hataponya.

 

MAOMBI NI YA MUHIMU ZAIDI KULIKO NGUVU

Maombi ni ya muhumu zaidi kuliko nguvu. Nguvu ni ya muhimu lakini maombi ni zaidi ya nguvu.

  • Mtume yakobo alikuwa mtu mwenye nguvu lakini nguvu yake haikumsaidia ili asiuwawe.
  • Mtume Petro alikuwa mtu mwenye nguvu, lakini nguvu zake hazikumsaidia kwamba asitupwe gerezani.
  • Mtume Paulo alikuwa na nguvu lakini nguvu zake hazikumsaidia kwamba asikimbie, asiwekwe zaidi ya mara moa gerezani na asipigwe karibia kufa zaidi ya mara moja.

Yesu alisema nawapeni nguvu, lakini ile nguvu haiwezi kumzuia shetani kufanya uharibifu kwa kanisa. Na nguvu haimsaidii mtu asiwe mwongo, wala haimsaidii mtu asidanganywe, maombi jambo pekee linalopelekea kanisa kutembea katika kweli ya Mungu.

Maombi ndiyo pekee yanaweza kumshinda shetani, maombi ndiyo pekee yanaweza kulishinda kusudi la shetani katika maisha yako na yangu. Herode alimchukua Yakobo na akamuua, Yakobo aliyetembea na Yesu, Yakobo alieona nguvu za Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, Yakobo aliyekuwa katika mlima ambao Yesu aligeuka sura ambako alimuona Musa na Elia! Petro alikamatwa akatiwa gerezani pamoja na nguvu zao.

Kilichomwokoa Petro ni maombi ya kanisa. (Matendo 12:1-5). Yakobo aliyemjua Bwana Yesu na alitembea naye aliuwawa kwa Herode.

Herode aliamini kuwa hata Petro, lakini cha ajabu kanisa likaingia kwenye maombi, yale maombi yakapelekea Mungu kuleta malaika na kuokoa kifo cha Mtume Petro.

  • Pasipo maombi nguvu ya Mungu maishani mwangu inaweza kupotea.
  • Pasipo maombi hata ahadi za Mungu kwangu zinapotea.
  • Pasipo maombi ni rahisi kupoteza mwelekeo.

Mathayo 7:7 “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; 8 kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? 10 Au akiomba samaki, atampa nyoka? 11 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?

Umasikini na nguvu chache za wana wa Mungu zinaelezewa kwa mapana na Yakobo kaka yake Yesu, si yule Yakobo mwana wa Zebedayo (huyu aliuwawa na Herode).

Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!”

Huna kitu kwa sababu huombi. Kuomba si tu kupiga magoti na Kuongea maneno yasiyo na maana. Mungu Anataka tufanye maombi yanayotoka ndani ya mioyo yetu. Maombi lazima yatoke ndani ya mioyo kwa kumaanisha. Ndiyo maana akasema Omba, Tafuta na bisha.

Najua shetani haogopi upako wangu au wako, anaogopa sana anapomuona Mtakatifu kapiga magoti na kuita BABA. Haogopi miujiza ufanyayo, haogopi vile nahubiri vizuri, haogopi utajiri wako, haogopi umbo lako, anaogopa unapopiga goti na kumuomba Mungu.

Unapoona huna nguvu na unapungukiwa na vitu sana, ujue wewe si mwombaji. Huwezi kuacha dhambi fulani au kuishinda, au kuikataa kabisa ni kwa sababu huombi. Huwezi kuacha dhambi na kushinda mpaka umepiga magoti na kuomba. Ni maombi pekee yanaleta nguvu maishani mwako.

Matendo ya Mitume 2:42 “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.”

Si tu kuomba bali ni kudumu katika maombi. Hii ina maana kwamba unakuwa hujisikii kuomba lakini unaamua kuomba. Unaomba muda ule mwili wako unajisikia uchovu mwingi sana. Ni kuomba wakati ule familia inasema baba/mama tunahitaji muda wako. Maombi huja kabla ya kuangalia familia. Omba omba, maana unapoomba utajikuta unaweza kutunza familia, utajikuta unaweza kunitunza familia na unapoomba lazima Uponyaji utoke katika familia yako.

Yeremia 33:3 “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”

Hapa anasema niite, naye ataitika. Si kwamba ataitika malaika au nani ni yeye baba wa Mbinguni. Sababu ya kwa nini Sauli hakupata msamaha wa Mungu ni kwamba hakuomba msamaha kwa Mungu alikumbuka kuomba msamaha kwa Nabii Samweli, Mungu hakumsamehe Sauli kwa sababu hakumuendea Mungu, akamwendea mwanadamu. Dhambi ya Daudi ilikuwa kubwa sana kuliko sauli lakini Daudi alisema Mungu Nisamehe na Mungu akamsamehe.

Isaya 1:16-19 “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; 17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. 18 Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. 19 Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;”

Unapokuwa na shida usiende kwa mwanadamu, nenda kwa Mungu.

Zaburi 50:15 “Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.”

Isaya 40:31”Bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Kama unasema uko bize kuomba jua uko bize kupata upako. Nimegundua kuwa maombi yanaweza kufanya kila kitu ambacho Mungu anaweza fanya. Nimegundua maombi yanaweza kufanya kile tu Mungu anaweza kufanya. Na kwa kuwa Mungu anaweza kufanya kila kitu basi maombi yanaweza kufanya kila kitu.

2 Korintho 6:18 ”Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike.”

Sasa tukitambua siri hii ya kuwa YEYE ni BABA na wewe u mwana ndipo lile Neno la Mathayo 7:7 ukilifanyia kazi majibu huja. Na matokeo yake ni Zaburi 107:20.

Unaona Nini?

Maandiko yanatuambia katika  Biblia Takatifu

Mith 23:7a “Aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo”.

Je wewe unaona nini mbele yako? Siku zote huwezi kuona kwenye moyo wako tofauti na kile unachokula kwa kusikia, kutazama ama kuhisi

Hii ndio sababu ninashauri watu wajifunze kuwa na vitu positive wanavyojishugulisha navyo kila siku kwenye maisha yao, maana kama wewe unasikia mambo ya mauti, unaona mambo ya mauti, unahisi mambo ya mauti ni rahisi kuota hata umekufa au uko kwenye jeneza ukasema nguvu za giza kumbe nafsi yako imejaa ayo mambo .

Marafiki wanaokuzunguka wanajaza nini kwenye nafsi yako, maana wanachokijaza kitakuwa na mchango mkubwa katika mtazamo wako kimaisha , mazingira yanayokuzunguka yanajaza nini katika nafsi yako, filamu unazo anagalia zinajaza nini, nyimbo unazo sikiliza mara kwa mara zinajaza nini katika nafsi yako, maana kama unakaa na watu waliokata tamaa uwe na uhakika hata maisha yako yatakuwa ni ya kukata tamaa tu.

Kama wewe ni mwana ndoa na mda mwingi unautumia kukaa na walioachika unaweza ukajikuta umeanza kubadilika kimtazamo, Ndio sababu Biblia ikasema katika;

1 Timoth 4:16 “Jitunze nafsi yako na mafundisho yako…”

Unajitunzaje ni kwa kuwa makini na vitu utakavyokuwa ukiviruhusu kuingia katika nafsi yako, kumbuka kuona kwako, kesho yako itategemea nini unakipa nafasi katika nafsi yako leo.

Jina Lake Tu

2 Wafilipi 2:10 “ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;”

Kiu na mpango wa Mungu ni kuona kila mwana wake aweze kutoa huduma ya Ukombozi. Ndiyo maana anasema

Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;- Marko 16:17

Anataka sisi tuishi kwa mamlaka yake huku duniani, ili kwamba kama mapepo yanazuia maisha, hatma na maendeleo ya mtu yeyote, yanapompata yeyete kati yetu, yaweze kukimbizwa. Ingawaje ni waamini wachache sana wanaoweza kufanya haya.

Mwamini yeyote anayetaka kufanya haya ambayo Mungu anatamani tufanye ya kufukuza mapepo lazima awe na ufahamu na Mkombozi Mkuu- Bwana Yesu. Kwa kadri unavyozidi kusogea kwa Yesu ndivyo upatavyo neema ya kukua kiroho na kuweza kufukuza mapepo, kumponya wagonjwa, kufufuka wafu na zaidi, Biblia inasema “Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.”

Mambo Gani Unahitaji Kuyajua Kuhusu Yesu? Unahitaji kujua nguvu iliyo katika jina lake. Neno linatuambia Bwana Yesu ana jina ambalo kila goti linapigwa kwake. Hatari ya hapa ni kwamba wengi sana wanaanguka maana Wakisha hudumia watu na kuona pepo yanawatii kwa kuonja nguvu za Roho Mtakatifu wanaanza kujiinua badala ya kumwinua Bwana. Wanafika mahali pa kutaka kukimbiza mapepo kwa majina yao. Tumeagizwa kukimbiza mapepo kwa Jina la Yesu tu na si jina lingine hivyo utajikuta katika matatizo mazito kwa Mungu na mapepo yenyewe. Unapoanza kutoa mapepo kwa jina lako unakuwa Yesu mwingine na unahubiri injili nyingine. Elewa kuwa kitendo hiki kimebeba laana

Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.” Wagalatia 1:9.

Hata mtume Paulo na upako wote aliokuwa nao aliendelea kufukuza mapepo kwa Jina la Yesu

Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.” Mdo 16:18.

OMBA: BABA, nipe Ufunuo katika maarifa Yako, nilishe mkate wa mbinguni ili niweze kukua katika ukomavu wa kiroho katika Jina la Yesu.

Mtoto Lazima Akue

Mathayo 28:18-20.

Hapo Tunajifunza juu ya AGIZO KUU LA YESU KWA KANISA.

Kwenda, Kusababisha, kuwabatiza, kuwafundisha ndipo ile mamlaka wataiona ikitenda kazi siku zote pamoja nao. Yesu yupo hayo yakitimizwa nasi. Ndipo tutafurahia wokovu wetu hapa duniani.

2 Petro 3:18 “Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.”

Mpango wa Mungu ni kwamba watoto wakue na kuwa wana. Kwa namna gani mtoto wa kiroho anaweza kukua na kuwa mwana?

1 Petro 2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”

Hili ni eneo ambalo linaleta changamoto sana katika kanisa la leo maana wengi wanakataa mafundisho wa kukulia wokovu. Ama wazazi wa kiroho wamejua kuzaa tu lakini watoto wana njaa kali na kuugua kwashakoo. Mtume Petro anaweka wazi Ukweli kwa mtu asiyejifunza na kukomaa kiroho ni kazi sana kumshinda shetani. Cha kushangaza akawa amezungumzia nyaraka za Paulo ambazo ni ngumu kueleweka kwa mtu asiyekaa darasani na kujifunza. Hivyo wengi wasioelewa nyaraka za Paulo wakajituka wanasoma na kuyachukulia mambo kijuu juu sana na kutohoa andiko kama lilivyo.

Matendo 2:41-43 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. 42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume.”

Waabuduo Katika Roho Na Kweli

Yohana 4:24 “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

https://www.facebook.com/efathambinga
Wana wa Mungu wakimfanyia Mungu wao Ibada.

Si matendo yote ya ibada ambayo Mungu anayakubali, kwa sababu si wote wamwabuduo ni waabudu halisi. Ukweli huu ulifunuliwa na Yesu alipokuwa anafanya mazungumzo na mama Msamaria katika kisima cha Yakobo. Alifunua pia ukweli mkubwa juu ya ibada ambayo tunatakiwa kuzingatia sana endapo tunataka ibada yetu ikubalike na Mungu.

Jambo la kwanza kuelewa ni kwamba kila “Mungu” ambaye anapatikana eneo fulani tu si Mungu wa kweli na hatakiwi kuabudiwa. Ibada inayofanyika kwa Mungu wa namna hii ni ibada feki. Ibada ya Mungu wa kweli haihusiani na kwenda njiapanda ambapo barabara tatu zinakutana kuweka chakula ili Mungu aje ale. Mtume Paulo alikutana na waabuduo namna hii katika milima ya Mars huko Athene (Matendo ya Mitume 17:22-31). Mungu wa Kweli anaelezewa na Mtunzi wa Zaburi katika Zaburi 8:1

Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;”

Ukweli mwingine ambao Bwana Yesu alitufunulia ni kwamba mungu yeyote ambao hana mahusiano ya ubaba na waabuduo huyu hastahili kuabudiwa nasi. Mtu yeyote anayemwabudu Mungu kwa namna hii si mwabudu halisi. Ndiyo maana Yesu alikuja kutufanya sisi wa Baba Yake. Na hata alipokuwa anawafundisha wanafunzi wake namna ya kuomba, alimwelezea Mungu wa kweli kama “Baba” (Luka 11:2). Zaidi sana, Bwana Yesu alitufunulia kuwa ibada yetu kwa Mungu si halisi kama hatumjui Mungu tunaye mwabudu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo kuwatambulisha watu wa Athene kuwa walikuwa wanaabudu kwa ujinga (Matendo ya Mitume 17:23). Alijaribu kuwafundisha kwamba ni kosa kumwakilisha kichwa cha Mungu na dhahabu, fedha, au jiwe lililo chorwa kisanaa na vitu vya kibinadamu (Matendo ya Mitume 17:29). Hakuna mwabudu ambaye kwa ujinga akafikiri kuwa Mungu Mtakatifu atakubali ibada toka kwa mtu ambaye maisha yake yametawaliwa na dhambi za uongo, kujifanya na kila aina ya maadili mabaya na uovu.

Ibada ya kweli inahusiana na kumwabudu Mungu wa kweli katika roho na kweli. Lazima tumwabuduo Mungu katika roho kwa sababu Mungu ni Roho, na ni kwa roho pekee tunaweza tukaendana na Roho Yake. Kumwabudu Mungu katika roho ina maana kufanya kile anachokuagiza ufanye katika akili ya kiroho ya imani. Kuna mambo ambayo Roho Mtakatifu wa Mungu angetaka sisi tufanye lakini tungeliona kwa macho yetu ya kimwili, ni magumu kuyaelewa. Kwa mfano, pale Mungu alipo muagiza Nuhu kujenga safina kubwa sana katika nchi kavu, kwa watu wa kizazi chake, hili halikuwa jambo lenye maana la kulifanya. Kwamba mtu lazima awe na mme au mke mmoja “haijarishi pana ubaya au wema” watu hawaoni umuhimu lakini ndivyo Mungu wetu atakavyo katika Neno lake. Mwabudu halisi hataweza kusema uongo hata kama kuna madhara yanayoweza kumpata kupitia Ukweli wake. Kwa mwabudu halisi kuwa mkweli si kwa ajili ya mtu bali kwa Mungu ajuaye yote.

Yohana 4:21-24 “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Ombi la Msingi: Baba neema ya kuishi maisha yanayokunalika kukuabudu wewe kupitia Roho Mtakatifu wako, katika Jina la Yesu.