KUJITAMBUA (SELF-AWARENESS).

Jitambue
Jitambue mwana wa Mungu

Kujitambua ni hali ya mtu kujifahamu yeye mwenyewe au utu wake. Hii ni kuwa na mtazamo wa wazi wa utu wako, ikiwa ni pamoja na uwezo, udhaifu, mawazo, imani, misukumo, na hisia zako. Kujitambua kunakupa kuelewa watu wengine, jinsi gani wanakuona wewe, mtazamo wako na majibu yako kwao katika wakati husika.

Tunapokuja mbele za Mungu lazima tuweze kujitambua Kuhusu hayo yote, ili tujue wapi tunakosea.

Kujitambua kunakupa kujua uendeje mbele za Mungu, maana pasipo kujitambua hutajua kama unabadirika, unaendelea ama la. Ukifika mahali pa kujitambua vipawa vyako na karama ndipo Unajua namna ya kufanya sawasawa na neema ya Mungu ndani yako.

2 TIMOTHEO 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.”

Siku utakapojitambua unahitajika uthamani wako unabadilika, umuhimu wa mtu haupo katika cheo chake bali kwa mamna unavyo hitajika, wangapi wanafaidiaka kutokana na wewe? Kila mtu anaye tambua umuhimu wake, anafanya vizuri kuliko wengine, ukijitambua utafanya mazuri kwa wazazi wako wakwe zako, unapotambua unahitajika utaitunza familia yako vizuri, na hili linatokea tu pale unapo baini kwamba jamii inauhitaji.

Kwanini unabadilika? Kwa sababu kuanzia saa hiyo wewe sio mali yako tena. Uthamani wako unakuja pale wewe unapojitambua kwamba wewe sio wewe tena, ila wewe ni wa wengine Huongei kwa sababu unataka kuongea bali unaongea kwa sababu kile unachoongea kina faida kwa jamii. Mtu aliyeokoka si mtu wa kawaida, ni mtu ambaye hajawahi kutokea duniani Kwa sababu umembeba aliyeumba mbingu na nchi Kupitia wewe lolote linaweza kutokea. Je? Wewe unafanana na mwingine? Hapana Basi ndipo unapoanzia utofauti na umuhimu wako.

Jitambulishe na onyesha umuhimu wako, Mungu hataenda kukuhoji mambo ya wengine bali atakuuliza umuhimu wako uko wapi? Wengine wanajidharau wanaona wao hawazezi bali wengine ndio wanaweza.

Huwezi kufanya vyema kama hujui jamii ina kuhitaji. Kuna mambo mengine hayahitaji elimu ya Darasani ili uyafanye Kama kumaliza chuo kikuu ndiyo akili tusingeona watu na mafaili wakizunguka kutafuta kazi wangefungua miradi na makampuni kwa elimu waliyopata ili waajiri wengine, Ingekuwa uprofesa ndiyo akili basi Tanzania ingekuwa mbali sana maana ina maprofesa wengi sana, lakini Tanzania bado ni maskini sana, Ingekuwa maprofesa wanafundisha vizuri tusingewaita watu waje kuchimba madini, mafuta na kununua nguo vitu mbalimbali kutoka china wakati vyote tunavyo.

WOKOVU. Daniel 3:16–17 “Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. 17 Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.

Kujitambua kuwa sisi ni wa thamani sana mbele za Mungu, kutatufanya tusicheze na dhambi. Mfano: Leo hii mtu anatenda dhambi lakini bado anaingia kwenye nyumba ya Mungu. Utaona kama unaendelea mbele na wokovu, kumbe Mungu alishakuacha siku nyingi.

Hawa vijana walitambua uthamani wao mbele za Mungu, ndiyo sababu hawakuwa tayari kuisujudia sanamu aliyoisimamisha Mfalme (Nebukadreza). Watu tusipoutambua uthamani wa wokovu tulionao tutakwenda mbele za Mungu ilimradi, tutaenda kwa mazoea ndiyo sababu mtu anaweza kuja Kanisani kwa muda anaotaka yeye. Waamuzi. 16: 20 “Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha.

Ukitambua kwamba umeokolewa kwa neema, utakuwa na wokovu wako binafsi wala siyo wa Wazazi au wa mtu mwingine. Mtu anaye shika maagizo ya Mungu anafananishwa na mwenye akili Kumbe ili uwe na akili ni lazima umpate mwanzilishi wa akili ambaye ni Mungu. Amua katika familia yako ikuone wewe ni wa muhimu kwao, hali kadhalika ofisini kwako katika huduma na popote pale ulipo jamii inayokuzunguka inakuhitaji.

Baada ya kutambua ndani yako nini tufanyeje?

Danieli 1:17 “Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto.

Uichochee Karama na huduma iliyoko ndani yako. 1Tim.1:6 “Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili

Uwe mnyenyekevu. Isaya. 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.

Uwe mtii. 1Thes. 5:12–13 “Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; 13 mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

Pamoja na vipawa na karama tulizonazo tuwatambue Viongozi na Watumishi wa Mungu ambao wanajitaabisha kwa ajili yetu. Ebr.13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi”.

Mtu mwingine akishaona kuwa ndani yake kuna huduma Fulani anaota kiburi anasema ni mimi tu ninayeweza, hii haifai.

FAIDA ZA KUJITAMBUA

  1. Utaleta msaada kwa watu wengine.Mwanzo. 45: 4 – 9 “Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. 5 Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. 6 Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. 7 Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. 8 Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri. 9 Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie.”  pia tunasoma Esta 4: 14 – 17 “Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? 15 Basi Est akawatuma ili wamjibu Mordekai, 16 Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie. 17 Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama vile Esta alivyomwagiza.” Ester alipotambua kwamba Mungu amemweka pale kwa makusudi yake alisema nitakwenda mbele ya Mfalme kinyume cha Sheria aliomba ikatokea.
  2. Utakuwa na ujasiri wa kuwaambia watu habari za Yesu. Rum. 1: 16 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” Leo hii mtu anafanya kazi mahali fulani na wale anaofanya nao hawajui kama ameokoka
  3. Hutatenda dhambi. Mwanzo.39:7–12“Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. 8 Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. 9 Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? 10 Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. 11 Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; 12 huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.” Zab. 119:11 “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
  4. Iko hatari kama hutatambua uthamani wa wokovu ulionao, watu wengine wameufanya wokovu kama mpira wanaurusharusha huku na huku. Mfano: Nguruwe ambaye amevalishwa pete ya dhahabu puani halafu anaidumbukiza kwenye tope. Mith. 11:22 “Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe
  5. Unakuwa na uwezo na mambo yote hata ya sirini; Dan 1:20, Dan 2:19
  6. Msimamamo
  7. Ujasiri
  8. Kijiamini
  9. Nidhamu
  10. Mahusiano mazuri na wengine.

MUBARIKIWE DAIMA

AMEN